Sambaza

BINTI KIBOKO YA ZARI KUTUA BONGO

NYOTA ya binti wa miaka 18, Regina Daniels maarufu kama ‘Kiboko ya Zari’ raia wa Nigeria inazidi kung’aa baada ya kuwepo kwa mpango wa kumleta Bongo, Risasi Jumamosi limewekwa wazi. 

Mpango huo unasimamiwa na muongozaji filamu maarufu nchini, William Mtitu ambaye ameliambia Risasi Jumamosi hivi karibuni kuwa michakato ya kukamilisha zoezi hilo unaendelea.

“Baada ya habari zake kutoka, nilivutiwa naye, nimemfuatilia binti huyo na kujiridhisha kuwa ni mtu maarufu na ana uwezo mzuri wa kuigiza filamu.

“Kuhusu utajiri wake mimi sikuangalia sana hilo, nilichoangalia ni namna gani naweza kumleta hapa nchini na kufanya naye kazi kama ilivyokuwa kwa Omotola (Omotola Jalade Ekeinde, msanii wa kike kutoka Nigeria) miaka ya nyuma,” alisema Mtitu.

MPANGO WASUKWA

Mtitu aliongeza kuwa amejaribu mara kadhaa kuwasiliana na binti huyo moja kwa moja ili kujua upatikanaji wake pamoja na gharama zake ameshindwa na kwamba sasa anatafuta mtu wa kumsaidia kufanikisha mpango wake huo.

Alisema: “Kuna tamthilia naisimamia inaitwa Rebecca inarushwa kwenye king’amuzi cha DSTV ni nzuri na ina mashabiki wengi sana. “Nimeona ili kuiongezea chumvi nimlete Regina tushirikiane naye,” alisema Mtitu.

REGINA NI NANI?

Kwa mujibu wa nyanzo mbalimbali mitandaoni, Regina ni binti wa Kinigeria ambaye alianza kazi ya uigizaji akiwa na umri wa miaka 6 na alipofikisha miaka 18, aliolewa na mfanyabiashara bilionea aitwaye Ned Nwoko ’59’.

Ndoa yake na bilionea huyo inatajwa kuwa imemfanya binti huyo mrembo kuogelea kwenye maisha ya anasa ambapo mbali na kuishi kwenye jumba la kifahari na kumiliki magari ya bei mbaya, anayo pia ndege yake binafsi.

AFANANISHWA NA ZARI

Kutokana na aina ya maisha yake wengi waliopata habari zake walimfananisha na Zari ambapo alibatizwa jina mitandaoni kuwa ni ‘Kiboko ya Zari’ kutokana na kile kilichotajwa kuwa amemzidi uwezo wa kifedha.

FILAMU ALIZOCHEZA

Kwa mujibu wa mitandao, Regina anatajwa kucheza filamu mbalimbali nchini Nigeria kama Dumebi in School, Python Girl, The Bat-Man na The Jericho.

Nyingine ni Plantain Girl, Jaja the Great, Tears of Ojiugo, Wipe your Sorrows na Royal Covenant ambazo zote alifanya vizuri.

MPANGO WA MTITU UTAFANIKIWA?

Katika mazungumzo na muongozaji wa filamu Mtitu, mwandishi wetu alijaribu kutia shaka juu ya nia ya muongozaji huyo kumleta Regina nchini kufanikiwa ambapo mwenyewe alisema:

“Hakuna kinachoshindikana, sitakuwa peke yangu katika hili nitawashirikisha na wasanii wenzangu kufanikisha hili. “Marehemu Steven Kanumba alifanikiwa kufanya kazi na wasanii wa Nigeria, kwetu sisi hiyo ni njia ambayo ametutobolea mwenzetu, tunatakiwa kuifuata,” alisema Mtitu.

HISTORIA KUJIRUDIA

Endapo Mtitu atafanikiwa kumleta binti huyo Bongo haitakuwa jambo geni kwani wasanii wengi wa Nigeria na Ghana wameshawahi kuja nchini na kufanya sanaa na baadhi ya mastaa wa filamu wa Kibongo. Wasanii nguli waliowahi kuja nchini na kushirikiana kikazi na wasanii wa filamu Bongo ni Omotola, Van Vicker, Emmanuel Francis, Mercy Johnson, Ramsey Nouah na wengine wengi.

TIMU ZARI WAHAHA

Tangu habari za Regina zivume na kupewa jina la Kiboko ya Zari, Timu Zari imekuwa ikihaha mitandaoni kumponda binti huyo kwa kusema hana alichompita Zari. “Kampita kwa hizo hela za mumewe, ujinga mtupu.” “Wanampa sifa za kijinga kumkuza kichwa mwisho kiwe kikubwa kama cha tembo.” “Zari atabaki kuwa juu halinganishwi na wanuka jasho.”

Baadhi ya komenti mitandaoni zikionesha kuwa Timu Zari haikubaliani na mtazamo wa Regina kumzidi uwezo wa kifedha. Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa mijadala hiyo imekuwa ikizidi kumpaisha chati binti huyo ambapo habari zake kwenye mitandao ya kijamii zimekuwa zikifuatiliwa sana na watu.

Toa Maoni Yako Hapa
#TUMESTUKA #NAWESTUKA! Pakua App Ya >>>255 Global Radio, Bofya Hapa

spotiXtra

jerseys wholesale Danton Heinen Jersey