Mrembo Wa Tanzania Alietwaa Taji China Afunguka
MREMBO Anitha Mlay aliyeshika nafasi ya pili katika Shindano la Kimataifa la Mazingira la Miss Landscape nchini China, amefungukia safari yake hiyo na shindano hilo kwa jumla. Akizungumza na SHUSHA PUMZI baada ya kutua nchini Jumanne iliyopita, alisema sababu zilizosababisha ashindwe kutwaa ushindi ni figisu zilizotawala kwenye shindano hilo.
“Mchujo wa awali uliwashirikisha warembo 17, lakini zikaanza fitna, tulipofika hatua ya nne bora ili kumpata mshindi, wasimamizi wa warembo wengine walionekana kuwa na maongezi ya faragha mara kwa mara na majaji, jambo lililoibua hofu kwa washiriki wengine,” alisema Anitha. Katika shindano hilo lililofanyika Juni 5, mwaka huu, mshindi alitokea Marekani ambapo alipata zawadi ya Dola 10,000, nafasi ya pili akachukua yeye – Anitha, ya tatu ikaenda Colombia.