Calisah Napenda Kuvaa Mitumba, Sivai Nguo Za Kariakoo
NI siku nyingine tena tunakutana katika safu hii ya My Style ambayo inazungumzia mastaa mbalimbali na kueleza maisha yao ya kila siku na vitu gani ambavyo hupendelea kuvifanya. Katika siku ya leo tunaye mwanamitindo maarufu ndani na nje ya nchi, Calisah Abdulhamiid ambaye kwa sasa anamiliki duka la kuuza viatu.
Calisah ni mmoja kati ya wanamitindo ambao wamefanikiwa kushiriki mashindano ya Mr. Afrika nchini Nigeria na kuibuka mshindi wa mashindano hayo mwaka 2018.
Leo My Style imefanikiwa kukutana naye na kupiga naye stori mbili tatu ambapo amefunguka mambo mengi zaidi usiyoyajua. Ungana nami…
My Style: Ratiba yako ya siku ikoje, ukiamka ni kitu gani cha kwanza huwa unaanza kukifanya?
Calisah: Huwa naamka saa mbili kamili asubuhi, kitu ambacho naanza kukifanya ni kusali, kisha nakunywa maji glasi nne kabla ya chochote. Baada ya hapo nafuatilia video za kuhamasiha kwenye Mtandao wa YouTube ndani ya nusu saa kwa sababu nimejiwekea ratiba ya kuangalia mbili kila siku, nikimaliza hapo ndio nashika simu yangu sasa kwa ajili ya mambo mengine.
My style: Unapendelea kwenda viwanja vya namna gani?
Calisah: Kwa kawaida mimi sio mtu wa klabu, kwa hiyo huwezi kunikuta nimehudhuria klabu yoyote kama sijaalikwa, hivyo mara nyingi wikiendi huwa napenda kwenda sehemu ambayo naweza kupata chakula kizuri tena huwa ni jioni.
My Style: Starehe yako kubwa ni nini?
Calisah: Napenda sana muziki, kuangalia muvi na sehemu kubwa ambayo huwa napendelea sana kwenda ni Mlimani City.
My Style: Wewe ni mmoja kati ya wanamitindo hapa nchini ambao una monekano mzuri na wa kuvutia watu wengi kwenye suala zima la mavazi, hebu tuambie ‘shopping’ zako huwa unafanyia wapi au una mbunifu wa mavazi ambaye huwa anakubunia?
Calisah: Kwanza sina mbunifu wa mavazi, lakini pia mimi sio mtu ambaye nanunua nguo kwa bei kali sana. Unajua vitu vingi ambavyo vinakuwa vya tofauti mara nyingi huwa vinapatikana sehemu ambazo watu wengi hawawezi kufikiria, kwa hiyo huwa sipendi sana kununua nguo ambazo kila mtu anazo kama nguo za Kariakoo. Nikitokea kuipenda sana nguo huwa nampa fundi ananishonea.
My Style: Matumizi yako kwa siku yanagharimu kiasi gani?
Calisah: Matumizi yangu kwa siku huwa haishuki 30,000 kwa sababu nina familia, naishi na mwanamke ndani na pia nina mtoto.
My Style: Ukiwa na stress ni eneo gani ambalo unapenda kwenda?
Calisah: Nikiwa na stress sikimbilii kwenda sehemu, huwa naangalia tatizo gani ambalo limenikuta, nikihisi nahitaji kupumzika kwanza huwa napenda kukaa ghorofani na kuangalia chini kwa sababu akili yangu ndio huwa inatulia kuweza kufanya vitu vingine kama kusikiliza muziki na kusoma vitabu vya akili katika maisha ambavyo ndani yake napata akili ya ziada. Lakini pia vitabu vya mambo ya fedha navyo vinanipa uelewa wa kutosha juu ya upatikanaji wa hela na elimu nzima ya kibiashara.
My Style: Kima chako cha mwisho kabisa kununua nguo na viatu ni kiasi gani?
Calisah: Sinunui nguo zaidi ya 300,000 na sinunui suti zaidi ya 500,000.
My Style: Nguo za mtumba unavaa?
Calisah: Ndio, nazivaa tena sana tu! Pia nimeanzisha kipindi changu cha Fall kinachofundisha watu suala zima la mavazi. Kipindi hiki ni kama tamthiliya ambayo ndani yake watu wanajifunza kuvaa.
Fall ni kipindi ambacho kinaonesha watu jinsi gani wanaweza kuvaa simpo bila machenicheni na wakapendeza, lakini pia kinawasaidia vijana wengi ambao wanapenda kujulikana kupitia mitindo.
My Style: Msanii gani Bongo ambaye mapigo yake yanakuvutia zaidi?
Calisah: Mtu ambaye naona anavaa vizuri na kila nikikutana naye naona anavaa ki-style sio mtu wakuko-complicate kwenye mavazi na huwa anavutia zaidi ni Izzo Business, anavaa vizuri sana, sio mtu wa michenicheni, sio mshamba na havai nguo za Kariakoo.
Tukija kwa wasichana kwa upande wangu ni Vanessa Mdee ‘Vee Money’ ni mjanja na anajua kuvaa we ‘mwenyewe si unaona mapigo yake sio ya kufananafanana yupo tofauti.
My Style: Unatembelea gari ya aina gani?
Calisah: Kwa sasa sina gari ila mwaka juzi nilikuwa natembelea Toyota IST na mwaka jana nilikuwa natembelea Klugger ni gari ambayo nilikuwa naipenda sana, lakini gari la ndoto yangu ni Toyota V8 naiwaza sana kwa sababu ni gari ambayo ukitokea sehemusehemu inaonyesha hadhi f’lan hivi.
My Style: Unatumia ‘perfume’ gani na bei yake ikoje?
Calisah: Natumia Tonford, bei yake ni 450,000 mpaka 500,000
My Style: Asante sana kwa muda wako!
Calisah: Karibu tena!
MAKALA: Memorise Richard