Sambaza

Maisha Ya Ben Pol Kufuru Aingia Rekodi Ya Diamond na Alikiba

WAKATI mwingine Mwenyezi Mungu anaweza kukuinua kutoka chini na kukuweka juu! Ndivyo ilivyomtokea staa wa muziki wa R&B Bongo, Benard Michael Paul Mnyang’anga ‘Ben Pol’ ambaye maisha yake kwa sasa ni kufuru kufuatia kumiliki mjengo wa ghorofa.

Kwa mujibu wa chanzo, Ben Pol tangu ameanza muziki maisha yake yalikuwa ya kati na kawaida, lakini kwa sasa yamekuwa supa na ni kama ‘amepindua meza’.

“Yaani nawaambieni siyo Ben Pol yule aliyekuwa akiishi Kijitonyama, Dar. Maisha yake yalikuwa ya kawaida tu ambayo anaweza kuishi staa wa kawaida anayeanza muziki, lakini kwa sasa hivi jamaa hashikiki kabisa kwani yupo mawinguni. Kwanza leo utamuona amekwea pipa ameenda nchi ile kesho nyingine, kote huko anakula bata,” kilisema chanzo.

MJENGO

Mbali na Ben Pol kuonekana akila bata la hatari hadi kuku wanaona wivu, jamaa anamiliki mjengo wa ghorofa moja ambao upo maeneo ya Mbezi-Beach jijini Dar. “Anaishi kwenye mjengo mkubwa wa ghorofa na huo anaumiliki yeye kama Ben Pol.

Aliamua kununua kwa sababu ya kurahisisha maisha hata akija na mpenzi wake wa Kenya (Anerlisa Muigai) mara kwa mara ambaye pia ana pesa chafu, basi awe anafikia nyumbani kwake.

“Sasa hivi ukifika kwenye mjengo huo utamuona tu Ben Pol anapenda kukaa juu kabisa ambapo kuna uwazi unaweza kumuona mtu yeyote anayepita barabarani,” kilifunguka chanzo hicho.

MAGARI KAMA YOTE

Ukiachilia mbali mjengo huo wa kifahari uliopo ushuani, Ben Pol pia amekuwa akionekana akiwa na magari ya kifahari likiwemo Mercedes Benz ML 350 (M-Class).

“Kimjinimjini anatembelea gari aina ya Mercedes Benz ML 350 (M-Class) jeusi hivi, lakini pia wakati mwingine hubadilisha kutokana na eneo analokwenda,” kiliweka nukta chanzo hicho kwa sharti la kutochorwa jina gazetini.

BEN POL AFUNGUKA

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Ben Pol anayekimbiza vilivyo na wimbo wake mpya wa Wapo kwenye YouTube alikiri kuishi kwenye mjengo huo na kwamba ni kweli mchumba’ke huyo akiwa Bongo hufikia hapo.

“Ni kweli naishi kwenye mjengo huo wa Mbezi-Beach (Dar) na mchumba wangu akija huwa anafikia hapo,” alisema Ben Pol kwa kifupi.

AINGIA REKODI YA MONDI, KIBA

Kutokana na kumiliki mjengo huo wa kifahari, Ben Pol anaingia katika rekodi ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye anamiliki mjengo Madale, Tegeta jijini Dar na Afrika Kusini huku akiwa amepangisha nyingine sehemu mbalimbali ndani ya Jiji la Dar.

Ben Pol pia anaingia kwenye rekodi ya staa mwingine wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ambaye anamiliki mjengo wa kifahari wa ghorofa moja uliopo Tabata jijini Dar.

Mbali na Wapo, Ben Pol ambaye ni zao la Nyumba ya Kukuza Vipaji (THT) ana nyimbo nyingine kali zilizompa umaarufu na shoo za kumwaga ndani na nje ya nchi kama Wakuone, Siyo Mbaya, Nikikupata, Bado Kidogo, Amen, Jikubali, Unanichora, Sophia, Samboira na nyingine kibao.

 

Toa Maoni Yako Hapa
#TUMESTUKA #NAWESTUKA! Pakua App Ya >>>255 Global Radio, Bofya Hapa

spotiXtra

jerseys wholesale Danton Heinen Jersey