Ndoa Ya Baraka The Prince, Najma Yanukia
WAKATI wakiwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu, hatimaye msanii wa Bongo Fleva, Baraka Andrew ‘Baraka The Prince’ amefunguka kwamba tayari yupo kwenye mipango ya kumuoa msanii mwenzake ambaye pia ni mpenzi wake, Najma Dattan na Mungu akipenda Agosti mwaka huu maandalizi yataanza.
Akizungumza na Risasi Vibes, Baraka alisema kuwa haoni sababu ya kutomuoa Najma kwa sababu ni msichana aliyekamilika kila idara, ana heshima, hana mambo mengi kama ilivyo kwa wasichana wengine, lakini sifa kubwa anayoipenda zaidi kutoka kwake ni mvumilivu na muelewa.
“Unajua mimi na Naj tumekaa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa kipindi kirefu sasa, hivyo sioni sababu ya sisi kuendelea kuwa wapenzi pia nimechoka kukaa naye mbali nataka nimuoe kabisa.
“Nataka nimuweke ndani kwa sababu ana kila sifa za kuwa mke wa mtu, kwanza ni mzuri, ana heshima, muelewa lakini kubwa zaidi ni mvumilivu, sasa kwa nini asiolewe?
Kwa hiyo natarajia Agosti mwaka huu ndiyo maandalizi ya ndoa yaanze ili ikibidi mwaka huu tuwe tumeshafunga ndoa tayari,” alisema Baraka.