Miaka 10 Ya Diamond Platnumz; Sio Rahisi Kuvaa Uhusika Wake
Amezaliwa Tandale, sehemu yenye sifa nyingi ambazo sio nzuri kuelezea kwa watu waliomfahamu kupitia mafanikio yake, ukweli pekee ambao hauwezi kupingika, Diamond Platnumz ni mzaliwa wa jamii ya watu masikini waliokataa kuishi kinyonge na kuamua kuutumia muziki kama daraja la kumvusha kuishi maisha ya kifalme.
Mwaka 2009 aliiachia ‘Nenda Kamwambie’ kama wimbo wake wa kwanza ambao ulimpa tuzo tatu ikiwemo ya msanii anayechipukia. Kamwambie ilifuatiwa na Mbagala, Nitarejea, Moyo Wangu na nyingine nyingi zinazoikamilisha miaka 10 ya Diamond Platnumz kwenye muziki wa Bongofleva.
Diamond amevunja rekodi nyingi za muziki ambazo hazikuwahi kufikiwa na msanii yeyote wa Bongofleva zikiwemo mauzo ya ringtones, kolabo na wasanii wa kimataifa , kuhudhuria na kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa na kujikusanyia tuzo nyingi za kimataifa.
Diamond anajulikana kwa majina mengi na hii ni kutokana na umahiri wake wa uimbaji na aina zake za uchezaji kwenye video zake ambazo zimekuwa zikiwaaacha hoi mashabiki wake.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Diamond amefanya vitu vingi kwenye muziki sambamba na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye nchi za Kimataifa.
Mbali na kuitangaza Tanzania, Diamond Platnumz ameweza kusaidia vijana wengine wengi wa kitanzania kupata ajira kwenye miradi aliyoainzisha baada ya mafanikio yake zikiwemo WCB na Wasafi Media.
Diamond ameweza kujikusanyia utajiri sio wa pesa pakee bali utajiri wa watu, kuna namba kubwa ya watu wanaelewa kinachofanywa na Diamond Platnumz na wapo tayari kumtetea kwa gharama yeyote kama ataonewa au kusemwa vibaya, haya ni mafanikio ambayo mtu yoyote anatakiwa kuwa nayo lakini Diamond Platnumz amezidi viwango. Chibu kama mwenyewe ambavyo anakuwa anajiita, amekuwa mwanamuziki mwenye mashabiki wengi TANZANIA kwenye akaunti zake zote za mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter, Facebook na Instagram.
Namfananisha Diamond wa Tanzania na Taylor Swift wa Marekani kutokana na heshima anayokuwa anaipata YouTube kila akiachia wimbo mpya, akiwa na zaidi ya video 500 zinazojumuisha nyimbo,interviews na tour zake kwenye YouTube Chaneli yake iliyofunguliwa Juni 12,2011, Diamond amefanikiwa kupata suscribers milioni 2.2 na views zaidi ya milioni 666 kitu ambacho sio rahisi kufikiwa na wasanii wengi wa Tanzania.
Katika kipindi cha miaka 10 Diamomnd amekuwa akiingia kwenye vichwa vya habari karibu kila siku ipitayo na hii ni kutokana na matukio yake ambayo kuna wakati sio rahisi kugundua kama ni uhalisia au ni maisha ya masupastaa.
Migogoro na wasanii wengine akitajwa kuwemo Alikiba na mahusiano mengi ambayo hakudumu nayo ni moja ya vitu ambavyo vimekuwa vikibeba ukubwa wa jina lake linapokuja suala la kutengeneza ‘headlines‘ kwenye vyombo vya habari.
Diamond ni baba wa watoto watano mwenye skendo ya kuzaa na wanawake tofauti wakiwemo Tanasha,Hamisa na Zari The Bosslady ambaye amezaa nae watoto wawili Tiffah na Nillan. Akiwa kama Baba anaetengeneza kesho bora kwa ajili ya watoto wake, Diamond amekuwa akifanya kazi nyingi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kusimamia makampuni yake na kuyatimiza majukumu yake kwenye muziki.
Miaka yake yote 10 Diamond ameachia single nyingi na Albamu mbili tu ikiwemo A Boy From Tandale iliyoachiwa mwaka 2018 na kusambazwa na Universal Music duniani kote, Kwenye “A Boy From Tandale’ Diamond ameungana na Omarion, Rick Ross, Psquare, Vanessa Mdee, Young Killer na wakali wengine wengi. Diamond ni balozi wa makampuni na taasisi tofauti ikiwemo mashirika ya ndege, vinywaji, na brands nyingine nyingi.
Akiwa kama msanii ambaye anategemewa kufanya kazi kwa ajili ya kuburudisha mashabiki wake, muda huo ni Boss ambaye anatakiwa kujua maendeleo ya miradi yake pia ni Baba wa watoto wengi ambao wote wanahitaji muda wake. Nadhani hiki ndicho kipengele kigumu zaidi kwenye maisha ya kila siku kwa mtu yeyote ambaye anaweza kujikuta kwenye uhusika kama wa Diamond Platnumz.
Licha ya kuwa anao wasaidizi lakini sio rahisi kuwa mtu mmoja ambaye unaweza kulisimamisha jina lako kama brand yako binafsi huku unategemewa kukagua miradi mingine na kupata muda wa kukaa na familia. Diamond ni Mkurugenzi wa makampuni matatu ambayo ni WASAFI MEDIA, ZOOM PRODUCTION na WCB.
Sio rahisi kuhakikisha michongo yote kwenye makampuni inaenda sawa wakati ambao tarehe za tour zimewadia na watoto wanatamani kuwa karibu na yeye, Kutokana na thamani aliyonayo, makampuni mengine hayaoni ajabu kufanya nae kazi ili kuongeza thamani ya bidhaa zao, Offa za matangazo zinamfikia wakati wowote bila kujua anapitia kitu gani kwa wakati huo.
Wakati ambao Diamond anafurahishwa na mashabiki wa uhakika wanaosaidia kuusukuma muziki wake bila kuacha hata siku moja, wapo ambao ni mashabiki wa uongo, watu wasiokuwa mashabiki na wenye chuki juu ya mwanamuziki huyu ambaye amekuwa akipata heshima kwenye nchi nyingi Duniani.
Mtindo wa maisha anayoishi wakati mwingine kuweka kila kitu wazi ni moja ya vitu vinavyomuongezea idadi ya watu wasiompenda, Kauli zake na vitu anavyoonyesha humfanya aonekane ni mwenye dharau na kujivunia kwa kila kitu alichonacho. Kama huo ni udhaifu wake kwa upande wa maisha yake ya kawaida sidhani kama ni sahihi kuhusisha na maisha yake ya muziki hadi chuki ichukue nafasi yake, Pamoja na yote Diamond ameweza kudhibiti chuki isiathiri muziki wake kwa kuendelea kufanya vitu vikubwa kila kukicha.
Diamond amekuwa msanii namba moja kwenye kila nchi Afrika Mashariki kwa muda mrefu bila kupoa, sio rahisi kwa msanii ambaye nyuma yake kuna wasanii wengine zaidi ya watano ambao wote wapo chini ya LABEL yake na Brand zao ni kubwa zinazohitaji gharama kuziendesha.
Diamond amekuwa msanii ambaye amekutana na changamoto nyingi kwenye muziki wake ikiwemo kufungiwa nyimbo zake na baraza la sanaa pamoja na baadhi ya vituo vya radio na TV kitu ambacho hakijawahi kumfanya asite kuendelea kufanya kazi zake katika mtindo ambao mashabiki wake wanataka kumsikia na kumuona.
Diamond hayachukulii mafanikio yake kama sababu ya kuuheshimu muziki peke yake bali kurudisha kwa jamii pia, Diamond amekuwa akionekana kuguswa na kusaidia wengine wenye mahitaji.
5,227 total views, 3 views today