Mtoto Miaka 9 Kuhitimu Digrii ya Uhandisi Umeme, Sasa Kusoma Udaktari, Phd
Jaribu kukumbuka wakati ukiwa na umri wa miaka 9 ulikuwa katika kiwango gani cha elimu? Jibu rahisi kwa wengi litakuwa ni elimu ya msingi hasa madarasa yale matatu ya chini.
Lakini hili ni tofauti kwa mtoto kutoka Ubelgiji afahamikaye kama Laurent Simons ambaye katika umri wa miaka 9 anahitimu masomo ya uhandisi wa umeme na kutunukiwa shahada ya kwanza ya masomo hayo.
Katika hali ya kushangaza kutana na mtoto Laurent Simons (9) ambaye amekuwa akisoma masomo ya Uhandisi wa umeme (electrical engineering) katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Eindhoven (TUE) nchini Netherlands yupo mbioni kuhitimu masomo hayo.
Masomo hayo ni moja ya masomo magumu katika chuo hicho jambo ambalo hata wanafunzi wa rika la makamo wamekuwa wakikiri ugumu wa somo hilo, lakini kwa Laurent hilo halikuwa tatizo bali aliendelea kubukua kitabu na sasa anakaribia kuhitimu.
Kwa mshangao mkubwa wafanyakazi wa chuo hicho wamekuwa wakistaajabu na kusema “Kama mchezo tu Laurent yuko tayari kuhitimu digrii yake mnamo mwezi wa kumi na mbili mwaka huu.”
Kisha ana mpango wa kuanza masomo ya PhD katika uhandisi wa umeme, Na kwa wakati huo huo pia anasomea digrii ya madawa, Baba yake aliongeza kwa kuuambia mtandao wa CNN.
“Hii sio kawaida,” alisema mkurugenzi wa elimu ya shahada ya uhandishi wa umeme kutoka chuo cha TUE, Sjoerd Hulshof. Laurent ni “wa kushangaza tu” Aliongeza Hulshof.
“Laurent ndiye mwanafunzi wa haraka sana ambaye tumewahi kuwa naye hapa,” “Sio tu kwamba yeye ni mwerevu zaidi, lakini pia ni mvulana mwenye huruma sana.” Alisema Hulshof.
Kiwango cha IQ ya mtoto Laurent inaelezwa kuwa ni IQ 145 ambapo ni asilimia 1 pekee ya watu duniani kote wanauwezo wa akili ya namna hiyo.
Laurent aliiambia CNN somo analopenda ni uhandisi wa umeme na pia “anasoma kidogo mambo ya medicine.”
Tayari Laurent anatafutwa na vyuo vikuu vyenye hadhi ya juu kote ulimwenguni kwenda kuendelea na masomo yake ya PhD, ingawa wazazi wa Laurent ( Lydia na Alexander Simons) hawajaweza kutoa tamko rasmi ni chuo gani wanafikiria kwa mtoto wao kwenda kufanya PhD yake.