‘BSS imebadilisha maisha ya vijana wengi’ – Madam Rita
Rita Paulsen almaarufu kama Madam Rita ambaye ni muanzilishi na Jaji mkuu wa shindano la kuibua vipaji vya kuimba Bongo Star Search (BSS) amefunguka na kusema kuwa shindano la BSS limefanikiwa kubadilisha maisha ya wasanii wengi waliowahi kushiriki au kupita katika shindano hilo.
Hii inakuja baada ya kuwa na tetesi mitaani kuwa wasanii ambao wanatoka katika shindano hilo huwa hawavumi wala kufanikiwa kwenye tasnia ya muziki licha ya kufanya vizuri katika shindano hilo.
Kupitia mahojiano aliyofanya na kipindi cha Bongo255 cha +255 Global Radio, Madam Rita ameweza kutengua kauli hiyo na kusema “Kila mtu atafanikiwa katika njia zake mwenyewe, sio kila mtu atakuwa kama Diamond au Vanessa Mdee. Hakuna mtu aliyewahi kupita BSS akawa na maisha ya kawaida wengi wamebadilika sana; Watu wanapenda kuongea vitu visivyo vya kweli ingekuwa vizuri wafanye utafiti kwa wasanii wote waliotoka BSS wako na maisha gani ndio waje na majibu ila wasanii wote waliopita BSS wamebadilika maisha yao kwa asilimia kubwa.”
Aidha aliongeza kwa kuwataja wasanii hao ambao ni Walter Chilambo, Haji Ramadhan, Kayumba, Frida Amani na wengine wengi ambao wamefanikiwa kutoka sehemu moja na kufika nyingine. Wote walifika BSS hakuna aliyewahi kuwafahamu kabla ila BSS akiwapa nafasi ya kufahamika na leo wapo kwenye jamii wanafanya vizuri zaidi. Alimalizia Madam Rita