Kamanda Mkondya: Uchaguzi 2020, Hatutapendelea Chama Chochote – Video

JESHI la Polisi nchini limesema limejipanga kwa kila kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu (2020), utafanyika kwa haki na amani huku jeshi hilo likiahidi kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi bila kupendelea chama chochote cha siasa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, januari 8, 2020 na Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi nchini, DCP Lukas Mkondya wakati akifanya mahojiano maalum na Radio namba moja ya mtandaoni nchini, +255 Global Radio, alipotembelea ofisi za Makampuni ya Global Group zilizopo Sinza Mori, Dar akimwakilisha IGP Simon Sirro huku akiambatana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, SACP Lazaro Mambosasa.

Katika ziara hiyo, Makamanda hao walitembelea vitengo mbalimbali vya makampuni ya Global Group kuanzia uzalishaji wa Magazeti Pendwa ya Uwazi, Amani, Ijumaa, Risasi Mchanganyiko, Risasi na Jumamosi, Global TV Online na Global Digital.

“Jeshi la Polisi hatupendelei CCM wala chama chochote kingine cha siasa, kazi yetu ni kusimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao, tunahakikisha sheria za nchi zinatekelezwa na kusimamiwa bila upendeleo. Ukifanya uhalifu tutakushughulikia bila kujali chama chako cha siasa.

“Tunafahamu mwaka huu tunakabiliwa na uchaguzi mkuu, tumejipanga vizuri, wananchi msiwe na hofu, kila mtu aendele akatekeleze haki yake ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi anayemtaka, kila mtu azingatie hali ya amani na utulivu. Uhuru bila sheria ni uendawazimu, tufuate sheria kwa utaratibu, ukifanya kazi nje ya hapo lazima tutakushughulikia.

“Tunapenda kutoa shukrani sana kwa wananchi wamekuwa wakishirikiana sana na jeshi la polisi kufichua mambo mbalimbali ya uhalifu. Polisi pekee hawawezi kufika kila sehemu, lakini wananchi wanafahamu maovu mengi yanayofanyika huko na wamekuwa wakitupatia taarifa na sisi tunazifanyia kazi na kuwakamata wahusika kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya haki ili sheria ichukue mkondo wake.

“Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni makosa ya ubakaji, mauaji, kujichukulia sheria. Sisi kama Jeshi la Polisi tumejipanga kutoa eimu kwa wananchi haya mambo wayakatae, wamrudie Mungu kwa dini zao ili waachane na haya mambo maovu kwa sababu ni kinyume cha sheria,” amesema Kamanda Mkondya.



