Global Radio Yasherekea Kutimiza Mwaka Mmoja – (Picha +Video)
WADAU na wafanyakazi wa Global Group Februari 7, 2020 wamejumuika kusherehekea mwaka mmoja wa redio ya kidijitali ya +255 Global Radio ambapo mambo yalikuwa pambe ile balaa. Hafla hiyo ilifanyika ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori, Dar.
Katika hafla hiyo wageni mbalimbali walijumuika na wafanyakazi na viongozi wa Global Group.
Miongoni mwa wageni hao alikuwepo msanii wa filamu nchini, Halima Yahaya ‘Davina’ na wenzake.
Katika hafla hiyo mambo yalianza kwa burudani ya muziki huku mshereheshaji na mtangazaji maarufu Bongo, Taji Liundi, akipambiza mchakato mzima.
Burudani zikiwa zimenoga, meneja wa radio hiyo ambayo inapatikana mtandaoni, Borry Mbaraka, alipata wasaa wa kuwakaribisha wageni na kueleza mambo kadhaa kuhusiana na radio hiyo.
Baada ya Borry, Mhariri Mtendaji wa Global Group, Saleh Ally, alieleza jitihada zilizofanyika kuifikisha radio hiyo hapo ilipo.
Abdallah Mrisho ambaye amekuwa akisifika kwa kuiongoza kampuni ya Global kufikia mafanikio ya kujipanua zaidi na kuanzisha miradi mbalimbali, naye alipata nafasi ya kuzungumza.
Mrisho alielezea jinsi alivyopewa wazo la kuanzisha redio hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo, na jinsi alivyoitafuta timu ya kufanya nayo kazi ambayo haikumuangusha mpaka sasa.
Mrisho alimsifu Borry maarufu kama The Pilot kwa jinsi alivyoipa redio hiyo maendeleo ya kasi kufikia kusikilizwa na maelfu ya watu ulimwenguni.
Baada ya Mrisho alifuata Shigongo ambaye aliwasifu wafanyakazi wake wote kwa uchapakazi wao ulioleta mafanikio ya radio hiyo na kampuni kwa ujumla.
Baada ya kutoa pongezi hiyo alikwenda kwenye studio za radio hiyo na kukata utepe kuashiria kuingia rasmi kwenye ushindani na kuahidi kuwa ndani ya muda mfupi ujao inatarajiwa kuwa radio tishio kuliko zote hapa nchini.