Sambaza

Stara: Kilimo kinalipa kuliko muziki

UWAZI limemtafuta msanii wa Bongo Fleva ambaye amewahi kutamba katika anga la muziki wa kizazi kipya miaka ya 2000. Huyu si mwingine bali ni Stara Thomas.

Wengi watakuwa wanamfahamu msanii huyu kutokana na nyimbo zake zilizobamba sana miaka hiyo na kumfanya kuwa staa wa kike aliyeipaisha vyema Bongo Fleva.

Stara ambaye ni mama wa watoto watatu, ameamua kuyaweka pembeni masuala ya muziki na kuhamishia majeshi kwenye shughuli za kilimo ambako anasema kunampatia riziki kuliko mambo ya kuimbaimba na kucheza majukwaani.

Uwazi: Umekuwa mwanamuziki wa zamani wa kike ambaye ulitamba sana kwenye muziki wa Bongo Fleva, nini kilikutumbukiza kwenye kazi hii ya sanaa?

Stara: Niliamua kuingia kwenye muziki wa Bongo Fleva kwa sababu niliona naweza na niliweza kwa sababu nina kipaji.

Uwazi: Hiyo ilikuwa zamani ila kwa sasa husikiki tena kimuziki, ndiyo kusema umeacha sanaa?

Stara: Kwa sasa masuala ya muziki siyo sana kama zamani kwa sababu nafanya vitu vingine tofauti na muziki ambavyo vinaniingizia kipato kinachonifanya niishi na watoto wangu pamoja na familia kwa ujumla.

Uwazi: Ni shughuli gani hiyo inayokufanya uishi na familia yako kiasi cha kuuweka kando muziki?

Stara: Siku hizi mimi ni mkulima, ndiyo maana hamnioni kwenye masuala ya muziki.

Uwazi: Umesema unalima, ni kitu gani ambacho unalima na unalima kwa kutumia jembe la mkono kama wakulima wengine?

Stara: Mimi ni mkulima wa mbogamboga kama mchicha, majani ya maboga, spinachi na nyinginezo. Kuhusu kulima silimi, mimi ila huwa nawaajiri watu wananilimia. Mimi kazi yangu ni kutunza na kusimamia.

Uwazi: Mashamba yako ya mboga yako wapi?

Stara: Nalima Mzenga mkoa wa Pwani na maeneo ya Veta mkoani Morogoro.

Uwazi: Unataka kuniambia biashara ya mbogamboga inalipa zaidi ya muziki?

Stara: Hii biashara ukiisimamia vizuri, muziki haufui dafu.

Uwazi: Kama nakumbuka vizuri, wewe ni mama wa watoto watatu?

Stara: Hahaha, ni kweli kabisa mimi ni mama yake Nikole, Jazz na Fareen.

Uwazi: Unaishi wapi na watoto wako?

Stara: Naishi nao nyumbani kwangu Tabata hapa jijini Dar es Salaam.

Uwazi: Habari za mjini zinasema kuwa mlitengana na baba wa watoto wako, ni kweli?

Stara: Si kweli, si kutengana tu lakini hata sijafikiria kuachana na mume wangu, niko nae tunakula minofu kama kawaida. Hao unaosikia wanasema tumeachana ndiyo wachawi wa maisha yangu.

Uwazi: Kuna mtoto yeyote ambaye amefuata nyendo zako za muziki?

Stara: Hakuna mtoto yeyote ambaye amefuata nyayo zangu, hata mimi sipendi wazifuate, napenda wajikite zaidi kwenye elimu kwani ndiyo ufunguo wa maisha.

Uwazi: Kwa hiyo kutokana na kujikita kwenye kilimo, unawaambia mashabiki zao kuwa wewe na muziki tena ndio basi au utaurejea?

Stara: Muziki kwa kuwa ushaingia kwenye damu siwezi kuuacha, hata hivi tunavyoongea nimeshatoa ngoma yangu inaitwa My Umbrella na hapa niko mbioni kukamilisha video yake.

Uwazi: Ule wimbo wako ulioimba na AT uitwao Nipigie, kolabo yenu ilinoga sana. Vipi kwenye hizo nyimbo zako zingine nazo umemshirikisha?

Stara: Hapana, jamaa sijamuona muda mrefu sana, nilipata taarifa kuwa kuna kipindi alikuwa Uingereza na hivi karibuni nimeambiwa yuko Marekani, ila mimi sina mawasiliano naye ya moja kwa moja.

Uwazi: Kwa hiyo hizo nyimbo zako mpya una matumaini kuwa zinaweza kukurudisha kama zamani utambe tena?

Stara: Kwa umakini mkubwa niliouweka kwenye nyimbo hizo, naamini nitarejea kwenye kilele cha muziki kule nilikokuwa zamani.

Uwazi: Vipi kuhusu Banana Zoro, bado ukaribu wenu kimuziki upo kama zamani?

Stara: Mahusiano yetu kimuziki yapo vizuri sana, hata sasa ninafanya kazi na bendi yake ya B-Band. Kwa hiyo tupo vizuri.

Uwazi: Nashukur u kwa mahojiano haya maalumu, nikutakie kila la heri kwenye shughuli zako za kilimo na hata huo ujio mpya kwenye gemu la muziki.

Stara: Asante sana, karibu tena.

Toa Maoni Yako Hapa
#TUMESTUKA #NAWESTUKA! Pakua App Ya >>>255 Global Radio, Bofya Hapa

spotiXtra

jerseys wholesale Danton Heinen Jersey