Manara: Kwa Uwekezaji Wetu, Ngumu Kuchukua Ubingwa Afrika – (Picha + Video)
MSEMAJI wa timu ya Simba SC, Haji Manara, leo Jumatano, Aprili 8, 2020 amefika katika ofisi ya Global Group zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam kufanya mahojiano na Global TV Online kuhusiana na masuala mbalimbali ya michezo na klabu hiyo yake juu ya usajili na safari yake ya Hispania.
Akifanya mahojiano na Global TV Online, Manara amesema wachezaji wa timu ya Simba kwa sasa wakitaka kufanya mahojiano na vyombo vya habari anatakiwa kuongelea maisha yake binafsi na sio kugusa timu ya Simba vinginevyo anatakiwa kuomba ruhusa kutoka kwa uongozi wa timu hiyo.
Pia ameongelea mchezo wao waliopoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, Uwanja wa Taifa akisema kuwa Yanga walicheza mechi hiyo kwa kupania sana ndio maana walipata ushindi na laiti kama wangekuwa wanacheza hivyo mechi zote za ligi wanagekuwa mabingwa lakini anashangaa wakikutana na timu ndogo wanafungwa kwa hiyo anaiona Yanga kama timu sawa na timu ndogo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumzia juu ya uwekezaji wa timu za Tanzania, Manara alisema: “Kwa uwekezaji wa sasa wa timu zetu nchini ni jambo lisilowezekana kuchukua ubingwa wa Afrika kwa aina ya wachezaji wanaosajiliwa na bajeti ya timu zetu kuwa ndogo.”
Pia amesema kwa sasa timu yao ya Simba inapata faida kutoka katika uwekezaji wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.