Sambaza

Mfugaji Aliyedaiwa Kuuawa na Askari TANAPA Azikwa

MFUGAJI Ulandi Dotto (28) mkazi wa Kijiji cha Mwanavala, Mbarali mkoani Mbeya, anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakati akipitisha mifugo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, amezikwa huku wafugaji wakishauriwa kutolipa kisasi.

Wafugaji pia wameombwa kutoichukia TANAPA kwa madai kuwa askari wanaodaiwa kufanya mauaji hao ni wahalifu kama wahalifu wengine na kwamba vyombo vya dola vinalishughulikia suala hilo.

Akizungumza wakati wa maziko ya kijana huyo yaliyofanyika kijijini kwao, Mwanavala Kata ya Imalilo – Songwe wilayani Mbarali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa, John Wambura, alisema chama hicho kitahakikisha haki inatendeka.

Wambura alisema akiwa kiongozi mkuu wa chama hicho, hatakuwa tayari kushuhudia wafugaji wakilipa kisasi dhidi ya askari waliotekeleza tukio hilo badala yake kila mmoja atatakiwa kuzingatia sheria.

“Mmesema hapa kwamba tukio hili ni la tano kutokea katika wilaya hii. Tunajua hakuna fidia ya uhai wa mwanadamu, lakini angalau serikali itoe kifuta machozi. Niwahakikishie kwamba hawa maaskari (askari) lazima mtawaona mahakamani,” alisema Wambura.

Alisema viongozi wa juu wa chama cha wafugaji nchini watahakikisha wanashirikiana na familia ya marehemu kuhakikisha haki inatendeka na familia inapata haki yake.

Baba mzazi wa marehemu, Mzee Dotto Shigela, aliwaomba wadau mbalimbali kumsaidia ili familia yake ipate haki kwa madai kuwa mtoto wake ameacha mke na watoto wawili ambao watahitaji kupata malezi bora.

Alisema Ulandi ndiye alikuwa mtoto wake wa kwanza na alikuwa msaada mkubwa kwenye familia, hivyo akadai kuwa maisha ya wanafamilia hao yatayumba kutokana na kutokuwapo kwake.

“Nililalamika kwa RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) maana walianza kupindisha wakati tunaandikisha. Walianza kudai kuwa risasi iliingilia kifuani wakati ukweli ni kwamba risasi iliingilia mgongoni na ikatokea kifuani, hivyo naomba sana haki itendeke kwenye tukio hili,” alisema Shigela.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambaye ni Ofisa Mifugo wa Wilaya hiyo, Augustino Lawi, alisema serikali inawathamini na inahitaji mifugo iendelee kustawi kutokana na kuwa miongoni mwa sekta zinazoiingizia mapato mengi.

Lawi alisema sekta ya mifugo ni ya pili kwa kuiingizia mapato halmashauri hiyo baada ya kilimo.

“Tatizo ni kwamba ufugaji wetu utategemea sana malisho ya asili kama wanyama wengine hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro. Sasa hivi tuna dhamira ya kubadili ufugaji kwa kuanza kuzalisha malisho ili tuondoe huu uhaba wa malisho,” alisema Lawi.

Mwanasheria wa chama cha wafugaji nchini, Glorious Luoga, aliwataka wafugaji kuhakikisha wakati wanadai haki, pia wazingatie sheria za nchi ili kuepuka migogoro isiyo na ulazima.

Alisema moja kati ya taratibu wanazostahili kuzingatia ni kuepuka kuingiza mifugo kwenye hifadhi na kwamba ni wajibu wa wafugaji kuzingatia utaratibu huo na kwamba hakuna haki bila wajibu.

Toa Maoni Yako Hapa
#TUMESTUKA #NAWESTUKA! Pakua App Ya >>>255 Global Radio, Bofya Hapa

spotiXtra

jerseys wholesale Danton Heinen Jersey