Amberr Washington Atua Global Radio, Kutoa Fursa Kwa Vijana (Picha + Video)
PRODYUZA ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Tuzo za Hollywood and African Prestigious (HAPA) kutoka Marekani, Amberr Washington, ametua ndani ya mjengo wa Global Group, Sinza-Mori jijini Dar na kueleza namna walivyojipanga kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji mbalimbali.
Akizungumza na +255 Global Radio, Amberr alisema kwa sasa tuzo hizo ni msimu wake wa tatu tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa mwaka huu wameona vijana wa Tanzania nao wana nafasi ya kushiriki.
Amberr Washington akipokewa na wafanyakazi wa Global Group.
“Wapo wasanii wachache kutoka Tanzania waliowahi kushiriki tuzo hizi akiwemo Rayvanny na Diamond. Mwaka huu tumetoa nafasi kwa vijana wote kwani lengo la kuanzishwa tuzo hizi ni kuwapa fursa vijana wa Afrika na Wamarekani weusi wenye vipaji vya kuimba, kucheza, kuandika mashairi, uanamitindo, kuigiza na vingine vingi.
…Akisani kitabu cha wageni.
“Jinsi ya kushiriki kama unajijua ni kijana una kipaji chochote kama nilivyoainisha, basi ingia katika website yetu ya www.hapawards.com na ujiandikishe bila kusahau kueleza kipaji chako ulichonacho. Kilele cha shindano hili ni Novemba 3, mwaka huu,” alisema Amberr.
…Akikabidhiwa gazeti na Mhariri wa Risasi Mchanganyiko, Andrew Carlos.
Amberr pia alikuwa ameongozana na balozi wa tuzo hizo nchini ambaye pia ni mmiliki wa Master Tanzania, Mawini Casy ambaye alizungumzia namna walivyojipanga kutoa fursa nyingine kwa vijana wa kiume wa Tanzania.
“Pia tumetoa fursa kwa vijana wengine wa kiume tu wenye vipaji vingi mbalimbali Agosti 2, (Ijumaa hii) pale King Solomoni, Namanga jijini Dar, tutawachuja na kuwapata watatu tu ambao watachukuliwa na HAPA na kupelekwa Hollywood, Marekani.
…Akifanya mahojiano na +255 Global Radio.
“Kule hatuwapi pesa bali tunawapa elimu. Katika hao vijana watatu watakaopatikana, kama watakuwepo wenye vipaji vya kuigiza basi watapata elimu kwa undani kuhusiana na tasnia hiyo chini ya waigizaji wakubwa, kama ni wanamuziki na hata wanamitindo nao watakutana na wabunifu wakubwa na kufundishwa,” alisema Mawini.
Aliongeza kwamba ili kijana achukuliwe katika kampuni hiyo ya Master Tanzania na kushiriki kuonyesha kipaji chake anatakiwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 29.
Balozi wa HAPA nchini Tanzania, Mawini Casy, akifanyiwa mahojiano na +255 Global Radio. “Awe ni raia wa Tanzania au mzazi wake mmoja. Asiwe ameoa na mwisho awe na kipaji chochote kile,” alisema Mawini.
Naye Ofisa Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Henry Mrutu, akielezea lengo la kuongozana na waratibu hao wa HAPA alisema:
Ofisa Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Henry Mrutu, akifanya mahojiano
“Tumekuja lisuala hili kwa upekee kwani kutakuwa na vijana wengi watakaojitokeza na kuibua vipaji na kuleta morali ya sanaa kwa kuongezeka wasanii wengi zaidi maana watu wengine wanalichukulia jambo hili kuwa ni la ujanjaujanja lakini kumbe limeleta watu kutoka nchi za mbali.
“Sisi kama Basata tutakuwa bega kwa bega na hili na hakutatokea kipingamizi chochote katika hili. Wasanii wajitokeze kwa wingi kadiri inavyowezekana ili chaguo liwepo la kutosha isionekane kama kuna watu wameshaandaliwa.”
Imeandaliwa na Andrew Carlos/GPL