Mtuhumiwa Mauaji ya Naomi Atishia Waandishi
IKIWA ndiyo siku ya kutajwa kwa kesi inayomkabili Hamis Luwongo anayetuhumiwa kumuua na kumchoma moto mkewe, Naomi Marijani, pameibuka taharuki katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakati Luwongo alipotaka kuwapiga waandishi wa habari kwa madai kwamba hataki kupigwa picha.
Tukio hilo la aina yake limetokea leo Jumanne, Agosti 13, 2019, mahakamani hapo alipokuwa akisubiri kuanza kwa kesi yake ambapo alijikuta akiinuka kwa nguvu kwenye kiti alichokuwa amekaa na kutaka kuwapiga waandishi, jambo ambalo lilizuiliwa na askari Magereza.
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo anaiomba itaje tarehe nyingine. Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Salum Ally, alikubaliana na shauri hilo la kuahirishwa ndipo mshtakiwa alinyoosha mkono kuiomba Mahakama azungumze jambo na Mahakama kumruhusu.
“Hakimu tangu nimefika hapa naona waandishi wa habari wamekazana kunipiga picha sana, yaani mpaka nimeingia humu ndani bado wananipiga picha tu bila kujua kwenye akili yangu nawaza nini, unajua mimi kwa sasa kichwa changu kimechanganyikiwa sana, hata hii kesi yenyewe sielewi itakuwaje.
“Nimekaa nitulize akili yangu halafu na wao wananisogeleasogelea kunipiga picha mwisho wanisababishe nifanye jambo ambalo si la kawaida, kwa sababu wanakuja hadi kunivua kofia jambo ambalo sijapenda,wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nitakuja kuishangaza mahakama,” amesema Luwongo mahakamani hapo.
Baada ya kueleza hayo wakili Simon alisimama na kujibu kwamba waandishi wanafanya kazi yao hivyo awape uhuru kwani wanazingatia sheria ya taaluma zao.
“Unajua mahakama zote hapa nchini zinakuwa na waandishi wa habari wanapiga picha na kutekeleza majukumu yao, hivyo naomba uwape uhuru wao, lakini kwa hilo ulilosema kwamba wamekuja mpaka kukufunua kofia ili wakupige picha sio kweli tena siamini kama wanaweza wakafanya hivyo.
“Kwa sababu wakati wanakupiga picha nilikuwepo na niliona tukio zima hawajakufunua kofia ila walikuwa wanakusogelea karibu ili wapate uso wako kwa kuwa ulikuwa umejifunika na kofia,” alisema Wankyo.
Kesi imeahirishwa hadi Agosti 27, mwaka huu kwa kuwa upelelezi haujakamilika.