Album ya Mwanadada Rapsody Kutumika Kama Somo Vyuoni
Rapa Rapsody aliachia album yake inayoitwa “Eve” mapema mwezi Agosti 2019, album ambayo ina maudhui ya harakati za mwanamke mweusi.
Miezi 8 baada ya album hiyo kutoka, vyuo viwili nchini Marekani “Ohio State University” na “University of North Carolina” vimeona ni vyema kuitumia kama somo ili kuwafundisha wanafunzi falsafa za harakati za wanawake wanaopambania haki za wanawake.
Kupitia ukurasa wake wa instagram, mwanadada huyo aliweka picha aliyoitoa kwenye ukurasa wa chuo cha University of North Carolina ambayo ilikuwa ikionyesha kuanzishwa rasmi kwa kozi ambayo inatumia album ya msanii huyo kusoma historia ya mwanamke mweusi toka karne ya 19.
Rapsody hakusita kuelezea furaha yake kwa kuandika “moja ya heshima kubwa ni kutengeneza kitu kwa ajili ya utamaduni na kisha kinatumika kama somo vyuoni, asanteni.”
Album hiyo ina nyimbo 14 na majina ya nyimbo hizo zote ni majina ya wanawake weusi waliofanya jambo kubwa kwenye jamii ya wanawake weusi Marekani kama Oprah, Aaliyah, Tyra, Michelle Obama na wengine wengi.