Msemaji Wa Serikali Afafanua Kilichofanya Tanzania Kuingia Uchumi Wa Kati
MSEMAJI Mkuu wa serikali, Dkt Hassan Abbas, leo Julai 02, 2020 amezungumza kuhusiana na Tanzania kuingia uchumi wa kati baada ya Rais Magufuli kutoa taarifa hiyo hapo jana.
Aliyoyasema wakati akiongea na wanahabari:-
Tunampongeza Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuweka rekodi ya tukio hili kutokea katika utawala wake, pia tunawashukuru na kuwapongeza Marais waliopita kwani wamefanya mengi yaliyochochea uchumi wakati wa utawala wao.
Miaka mitano kabla ya lengo letu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 nchi yetu imeweza kuingia katika uchumi wa kati lakini hii haina maana tuache kuchapa kazi. Nawasihi Watanzania tuendelee kuchapa kazi.
Uchumi wa kipato cha kati umehusishwa na nchi ambayo umasikini unapungua, uchumi imara unajengwa, uzalishaji viwandani unaimarika na wananchi wanapata maendeleo.
Uchumi wa kipato cha kati tulioingia umegawanyika katika sehemu mbili, uchumi huu unahesabika ikiwa pato la mwananchi kwa mwaka ni USD 1,036 hadi USD 4,045.
Misingi kumi iliyotusaidia kuingia katika kipato cha kati ni amani na utulivu, mipango thabiti ya maendeleo, utekelezaji usioyumba, kufanya maamuzi magumu,azma ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi.
Misingi mingine ni kuimarisha miiko ya uongozi, kuwekekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati inayokuza uchumi, kuwekeza kwenye maendeleo ya watu pamoja na kujenga sekta binafsi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa