“Waliandaa Mkakati Nitumbuliwe” – RC Makonda Afunguka Mazito
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameamua kuvunja ukimya na kuanika namna alivyotengenezewa mkakati ili afukuzwe katika wadhifa wake huo wa kuwatumikia wananchi wa Jiji la Dar.
Makonda amesema katika ibada ya Mkesha wa Tamasha la Campus Night lililofanyika usiku wa kuamkia leo katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe, Dar.
“Unganisha kusudi la Mungu kwenye maisha yako na digrii unayosomea, kuna watu hapa masomo ni magumu kwa sababu mnasoma masomo ambayo Mungu hakukuumbia, kwa hiyo hata ukimuomba akusaidie hawezi kufanya hivyo kwa sababu Mungu hajikorogi.
“Kama umeumbwa kuwa mfugaji nenda kasome SUA Morogoro, kama umeumbwa kuwa Mjenzi nenda kasome hapo ARDHI na kama umeumbwa kuwa Mhasibu, nenda huko IFM. Mungu amemuumba kila binadamu kwa kusudi lake. Huku kujikoroga mtamtesa mchungaji wala hamtafaulu.
“Nilipokuwa chuoni, mwalimu akifundisha, mimi simsikilizi kwa lengo la kufaulu somo lake bali kukamilisha uongozi wangu nikiwa kwenye madaraka na hili nililianza mapema. Nilikuwa nikimpigia simu Waziri wa Michezo wakati huo Mkuchika, nampa tip anazitendea kazi napata pesa, leo ninatumia uzoefu ule katika uongozi wangui.
Kuna watu wamejipanga usiku na mchana kuhakikisha sibaki kwenye kiti changu, nilipopata taarifa hizo nikamwomba Mungu. Nilipofika Ubungo wananipiga picha za kuniaga, nikachukua simu kuongea wakaanza kusema amepigiwa simu kuambiwa ametumbuliwa.
“Siku hiyo Rais magufuli alikuwa amechelewa kufika kwenye mkutano huo wakaanza kusema amechelewa kwa sababu alikuwa anakamilisha uteuzi wa Mkuu wa Mkoa atakayenirithi. MC akatangaza pale kwanza atakayempokea Rais ni Waziri wa Ujenzi, wengine wote akiwemo Mkuu wa Mkoa mkae msinyanyuke, wakaambizana, makonda kwisha habari yake, nikaenda kwa dereva wangu nikamkuta analia.
“Baadaye nikaitwa kutoa salamu za mkoa, nikamwambia Rais haijalishi wanagapi wanakuunga mkono, Rais akanyanyuka akanipa mkono, watu wakasema huo mkono ni wa kuagana naye, aliposimama kuongea akasema, “Makonda piga kazi”, ile dunia yote ikabadilika… Waliokuwa wamewaleta kuzomea wakifukuzwa wakaanza kulia na kugalagala.