Dully afichua Harmonize alichofanya Wimbo wa Nikomeshe
MUDA mchache baada ya kutinga katika viunga vya Global Group, Sinza Mori jijini Dar maalum kwa kutambulisha ujio wake mpya wa Nikomeshe, mkongwe katika gemu la Bongo Fleva, Dully Sykes amefichua namna Harmonize alivyohusika katika ngoma hiyo.
Dully aliyasema hayo leo mchana mara baada ya kupokelewa kwa shangwe na umati wa wafanyakazi wa Global Group na kupelekwa +255 Global Radio kuwa, amekuwa karibu na Harmonize kwa ajili ya kufanya muziki wa kibiashara.
“Katika wimbo wangu mpya na Harmonize wa Nikomeshe, ule kwanza sikutunga mimi, nilimwambia Harmonize tengeneza wimbo wote mimi nimeenda nimeimba tu. Kwa hiyo ni ubunifu tu,” alisema Dully Sykes.
Dully pia aliongezea jinsi anavyonufaika kufanya kazi na Harmonize.
“Ukiona Harmonize ameweka katika ukurasa wake wa Youtube ile ni kazi yetu wote. Vidole viko vitano unafikiri ukikata vinne kimoja kitakuwa na kazi gani? Shigongo wakati anafungua Global miaka ya 1999 kwanza kompyuta zenyewe zilikuwa hazipatikani na kulikuwa na ofisi ndogo tu ya watu wanne nakumbuka kwani nilikuwa mtu wa kwanza kufanya naye kazi.
“Leo hii nimeingia hapa (Global Group) nimeshangazwa kuona makampuni yameongezeka na kuwa mengi, watu wamekuwa wengi hata sikutegemea. Kwa kipindi kile Shigongo angeamua kufanya kazi kama zamani na watu watatu tusingemsikia leo hii, tusingeisikia +255 Global Radio wala chochote cha Shigongo lakini kwa sababu alitafuta watu wa kutafuta nao kazi na kuwalipa ndiyo maana yupo hapa leo hii.
Dully alimaliza kwa kuwashukuru wafanyakazi wote wa Global Group na mashabiki kwa kuonesha ushirikiano kila anapoachia wimbo mpya.
“Asanteni kwa sapoti yenu. Kufika na kupokelewa vizuri nimefurahi pia kwa kunipa nafasi kucheza ngoma zangu na pia mashabiki asanteni kwa kunikubali kila siku hamchoki, kwa kweli napendwa na watu hilo naomba niwashukuru.”
Kuyapata mahojiano kamili, tembelea Global TV Online katika Mtandao wa Youtube au ingia Playstore katika simu yako na tafuta +255 Global Radio utapata kusikiliza vipindi vyote vya kijanja mjini.
Imeandaliwa na Andrew Carlos/ GPL / Picha na Richard Bukos